jump to navigation

Waziri SMZ azidi kulikoroga September 26, 2009

Posted by zenjmedia in Uncategorized.
trackback

• Baada ya kuwashukia Wamarekani, sasa awageukia Watumbatu

• Azidi kuiharibia SMZ kwa wananchi wa Zanzibar na Jumuiya za Kimataifa

Na Waandishi Wetu

Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi wa SMZ,na Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura Wilaya ya Mjini Unguja Hamza Hassan Juma,ameibuka tena kwa kutoa kauli zenye utata ambazo zinazidi kuiweka pabaya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mbele ya jumuiya ya wananchi wa Zanzibar na dunia kwa ujumla baada ya kuwaambia wananchi wa kijiji cha Tumbatu  Jongowe kuwa hawana akili kwa vile wengi wao hawakusoma, na kupelekea wananchi hao kugoma kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.

Waziri huyo ambaye ameibuka hadharani kutoa matamshi mazito yanayozidisha chuki kwa baadhi ya wanajamii hasa baada ya kuihukumu Serikali ya Marekani kuwa inahusika katika kuihujumu SMZ huko kisiwani Pemba katika uandikishwaji wa dafari la kudumu la wapiga kura, mara baada ya Serikali hiyo ya Marekani kuwataka wananchi wake kuchukuwa tahadhari kutokana na kuwepo dalili za kutoweka kwa amani kisiwani humo, hali ambayo inazidi kuipa wakati mgumu SMZ,katika jumuiya za kimataifa.

Wakati sakata hilo bado halijatulia vyema, Waziri Hamza ameibuka upya kwa kauli zake zenye utata,kwa kuwaambia wananchi wa Tumbatu hawakusoma,katika sakata linalolalamikiwa la mgogoro wa Ardhi, hivyo kuzusha hisia za chuki baina ya wananchi na wakaazi wa mji huo, ambao wameamua kujiunga pamoja na kugomea uandikishwaji katika daftari la kudumu la wapiga kura na hata kubadishiwa shahada hizo, huku mgogoro huo ukiweka mbali itikadi za kisiasa, baada ya wanachama wa CCM na CUF kuungana na kugomea zoezi hilo.

Msimamo huo wa aina yake kuwahusisha wanachama wa CCM na CUF umeelezewa kuwa ni kuipelekea ujumbe Serikali juu ya madai yao ya kunyanganywa ardhi wananchi kijiji cha Jongowe na kupewa wananchi cha kijiji cha Kichangani, ambapo Wananchi wa eneo hilo wamesema licha ya mgogoro huo pia wamekasirishwa na kauli ya Mhe. Hamza Juma aliposema wananchi wa Jongowe hawana akili kwa vile wengi wao hawakusoma kitendo ambacho kimeonekana ni cha kuwazadharau.

Akizungumza na ‘Nipe Habari’,wakala wa CCM ambaye amekataa kutajwa jina lake gazetini kwa sababu za kiusalama amesema kuwa wameamua kuweka mgomo huo hadi pale viongozi wa juu watakaposikiliza matatizo yao na kuyapatia ufumbuzi kwa kurejeshewa ardhi yao,ili wasitishe mgomo huo,ambao unazidi kuiweka pabaya SMZ kutokana na kauli za baadhi ya mawaziri wake.

Pia amesema wamedharauliwa na kiongozi huyo wa Serikali hivyo wanaungana na wenzao wa kijijini hapo kugomea zoezi hilo kwani wameambiwa kura zetu 350 hazisaidii kitu katika serikali “Pia Serikali ya mkoa imeshindwa kututekelezea mahitaji yetu na sisi jambo lolote linalokuja la kiserikali hatutolikubali hili ni suala la kijamii si suala la vyama, kwa kuwa wanatudharau kuwa ni wachache,sasa tutaionyesha Serikali kuwa sisi hatutaniwi,na kila anayetudharau na sisi tunampuuza” amesema wakala huyo na kuongeza;

“Mgomo huu ni wa pamoja baina ya CCM na CUF ambapo kwa upande wetu CCM nasi tumedharauliwa na kiongozi huyo wa Serikali hivyo tunaungana na wenzetu kijijini kugomea zoezi hilo” alisisitiza wakala huyo.

Katika kuonyesha kuwa mgomo huo umeitikiwa na wanakijiji hao, suala la uandikishwaji limekuwa halina mafanikio kabisa tangu zoezi hilo lianze Septemba 21,baada ya kutoandikishwa hata mtu mmoja katika daftari hilo la kudumu,hali inayozidi kuiweka pabaya Serikali ya SMZ kufuatia kauli za baadhi ya mawaziri wake,ambao wamekuwa wakionyesha kuwa na kauli za dharau zilizojaa kebehi.

Katika kulifuatilia suala la uandikishwaji katika daftari hilo,Mkuu wa kituo cha uandikishaji Suluhu Ali Rashid amesema tokea kazi hiyo ianze mnamo Septemba 21 hakuna hata mtu mmoja aliyeandikishwa kituoni hapo,ambapo alipobanwa na gazeti hili kujaribu kubainisha chanzo cha uzorotaji wa uandikiswaji wa katika daftari hilo ambalo pia litatumika katika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wawakilishi mwaka 2010,aligusia kuwepo uwezekano wa kugomea zoezi hilo.

“Huu unaweza kuwa ni msimamo wa wanajamii kwa pamoja nadhani wamedhamiria kuiadhibu Serikali kutokana na madai yao hayo ya kunyang’anywa ardhi yao wananchi wa kijiji cha Jongowe na kupewa kijiji cha Kichangani, hali hiyo imesababishwa na kutoridhika na maamuzi ambayo yametoka kuhusu mzozo wao ndio iliyosababisha kijiji kizima kushikamana pande zote mbili.

Katika jitihada za Serikali ya SMZ kujaribu kuwashawishi wananchi hao kujiandikisha,Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pembe Juma Khamisa amewataka wanakijiji hao kuchukua hatua ya kujiandikisha kwanza wakati suala lao serikali inalishughulikia na kuahidi kulipatia ufumbuzi,huku akiwaasa kuwa daftari lina mwisho wakigomea watakosa haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka .

Waziri Hamza hivi karibuni alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imedai fujo zinazoendelea hivi sasa kisiwani Pemba ni mpango maalumu na wa muda mrefu wa serikali ya Marekani.

Kauli hiyo ya kulishutumu taifa kubwa duniani iliitoa Waziri huyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo cha uandikishaji cha shule ya Sizini mkoa wa Kaskazini Pemba. Mwishoni mwa mwezi uliopita, Marekani ilitoa taarifa kwa raia wake ikiwataka kuwa makini na safari za kisiwani Pemba ambako ilisema kuna vurugu zinazohusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Marekani, ambayo ina tabia ya kutahadharisha raia wake kufanya ziara sehemu ambazo kuna ama kunaweza kutokea vurugu, ilieleza kuwa tangu kuanza kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura, kumekuwa na vurugu kubwa kisiwani Pemba na kuwaonya raia wake kuwa makini na mikusanyiko wawapo visiwani Zanzibar, huku ikiwataka wajiandikishe kwenye ubalozi wake mara watakapowasili Tanzania.

Lakini SMZ ilijibu vikali taarifa hiyo ya tahadhari kwa raia wa Marekani na Waziri Juma alieleza msimamo wa serikali yake kuhusu kitendo hicho cha Marekani.

“SMZ inaamini kwamba Marekani ilikuwa inajua nini kitatendeka katika kisiwa cha Pemba na ndio maana ikaanza kutoa tahadhari kwa wananchi wake mapema,” alisema Waziri Juma ambaye alisema ametumwa na serikali kwenda Pemba kuangalia hali ya usalama.

“Haiwezekani Marekani iwatake wananchi wake wasitembelee kisiwa cha Pemba halafu iwe haijui nini kitatokea katika kisiwa hicho, alinukuliwa Waziri huyo ambaye amekuwa na hulka ya kutoa majibu ya kushtukiza.

“Sisi serikali ya Zanzibar tunaamini kwamba Marekani ndio iliyopanga mpango huu maalumu wa kufanyika vurugu huku Pemba na ndio maana wakawatahadharisha raia wake mapema wasitembelee Pemba. Kama walikuwa hawajui kwa nini watoe tahadhari? Wanajua na ndio waliopanga mpango huu kwa kutafuta sababu wanazozijua wao.”

Zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura kisiwani Zanzibar limekumbwa na vurugu kubwa na awali serikali ililazimika kulisimamisha baada ya wananchi kurushiana mawe na polisi.

Juzi polisi walilazimika kutumia silaha za moto kutawanya wananchi ambao walijikusanya nje ya vituo vya kujiandikishia kwa lengo la kuzuia wenzao kujiandikisha.

Tayari nchi 14 wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani zimeshaitaka SMZ kushughulikia matatizo yaliyojitokeza kwenye zoezi la uandikishaji wapigakura ili kuufanya uchaguzi ujao kuwa huru na wa haki. Tatizo kubwa linalopingwa na wananchi wa Zanzibar ni matumizi ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kama ndio sifa kuu ya mtu kuandikishwa.

Wananchi wengi visiwani Zanzibar, ambako mkaazi ni yule aliyeishi kwa miaka mitatu mfululizo, wanadai wamenyimwa vitambulisho vya ukaazi na hivyo hawawezi kuandikishwa kupiga kura. Waziri huyo pia alisema ili kuondokana na masharti ya nchi wahisani, SMZ itaanza kusimamia uchaguzi wake na kuachana na ufadhili wa wahisani kwa madai kuwa uzoefu unaonyesha kuwa ufadhili huambatana na masharti, jambo ambalo alisema si jema.

Kwa mujibu wa Waziri Juma, pamoja na kuwa nchi wahisani wanatoa fedha kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali, hakuna sababu ya nchi hizo kuingilia mambo ya ndani kwa kuwa kila nchi ina uhuru wake na inajiendesha.

Alisema fedha zinazochangwa na wafadhili ndio zinazosababisha matatizo yanayototokea Pemba sasa kwa kuwa wafadhili huwa wana masharti yao, hivyo SMZ itaanza kusimamia uchaguzi wake hata kama italazimika kuchangishana shilingi moja moja.

“Mtu akikufadhili ndio anakuwekea masharti anayotaka yeye lakini sisi wenyewe tutaanza kuchanga fedha wenyewe ili kusimamia uchaguzi wetu wenyewe maana tushaona hawa wanataka kutuletea maneno mengi,” alisema Juma. Waziri Juma alisema SMZ haitaki kuona fedha za wafadhili zinatumika kuvuruga amani na kwamba itatumia nguvu zake zote kurudisha amani iliyoanza kutoweka katika kisiwa cha Pemba.

“Sisi ni wasimamizi wa sheria… Marekani walikuwa wanajua nini kitatokea lakini tunasema tutatumia nguvu zote katika kurejesha hali ya amani kwa sababu tunajua hii ni mbinu tu na hatutaivumilia hali hii,” alisisitiza waziri huyo. Alisema pamoja na matatizo yote yaliyotokea, uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 utafanyika kama ulivyopangwa hata kama Zanzibar nzima wataandikishwa watu 100.

“Tunasema uchaguzi utafanyika na upo pale pale hata kama ni watu 100 wataandikishwa, hatutaacha kufanya uchaguzi kwa visingizio kama hivi kwa sababu hatutaki kufadhiliwa; uchaguzi ni wetu wenyewe,” alisema Waziri Juma. Alisema kuanzia sasa mtu yeyote au kiongozi atakayehamasisha wananchi kufanya fujo ili kuharibu zoezi hilo, atachukuliwa hatua za kisheria.

”Haiwezekani mwananchi anataka kutumia haki yake, halafu mwingine anamkataza kufanya hivyo. Kwa kweli kama tukimgundua kiongozi au mtu yeyote tutamchukulia hatua za kisheri kwa kuwa anachochea vurugu,” alisema Hamza. Alisema kuwa wananchi ambao bado hawajapata fursa ya kujiandikisha, watapata fursa wakati mwingine kwa kuwa zoezi hilo litafanywa kwa awamu tatu.

Kuhusu tatizo la vitambulisho vya ukaazi, Waziri Juma alikanusha kuwa ndilo lililosababisha kutokea kwa mvutano kati ya wananchi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) na kusababisha zoezi hilo la uandikishaji kugomewa.

“Vitambulisho ni propaganda za kisiasa tu ambazo zinafanywa na wafuasi na viongozi wa upinzani, lakini sisi tunasema tunatumia nguvu zote katika kuhakikisha tunamaliza suala hili. Wacha wao wagome lakini tutawaandikisha wanaotaka kujiandikisha,” alisema. Alisema hali hairidhishi lakini ameahidi kutumia nguvu za ulinzi katika kurejesha amani, na kudokeza kuwa fedha nyingi zimetumika katika kuimarisha ulinzi na usalama.

“Sitaki kusema ni kiasi gani tumetumia lakini nakwambia ni fedha nyingi sana tumeshatumia na tunaendelea kutumia kwa kuwa hilo si tatizo kubwa,” aliwaambia waandishi wa habari, hali ambayo inazidisha utata juu ya hatima ya uhusiano mwema baina ya SMZ na Serikali hiyo kubwa zaidi duniani.

Advertisements

Comments»

No comments yet — be the first.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: